Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa shilingi Bilioni 1.3 kutekeleza awamu ya kwanza ya Mradi wa Uboreshaji Upatikanaji wa maji eneo la NALA Jijini Dodoma ambao utawanufaisha wananchi 14,731 utakapokamilika.
Akiwa katika mwendelezo wa ziara ya kukagua Miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Mkoa, Rosemary Senyamule Leo Julai 23, 2024 amefika eneo la mradi wa maji NALA kufanya ukaguzi wa utekelezaji wa mradi huo.
Senyamule amemtaka Mkandarasi anayejenga mradi huo ( BAHAJ Construction company LTD) kukamilisha kazi aliyopewa na Serikali kwa wakati ili wananchi wa mitaa mitatu ya Nala Centre, Segu Juu na Chikoa kwa awamu ya kwanza ya Ujenzi wa mradi huu wanufaike na huduma ya maji.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imeanza utekelezaji wa mradi huo tangu Julai 01, 2024 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita.
Mradi wa maji NALA unahusisha Ujenzi wa tenki la kupokelea maji la ujazo wa lita 200,000, Ukarabati wa tenki la kupokea maji lenye ujazo wa lita 45,000, Ulazaji wa mtandao wa mabomba wa kilomita 7.8, Ujenzi wa Jengo la Pampu (Pump House) litalokasimikwa pampu mbili za kusukuma maji na Kuweka Mfumo wa kutibu maji.