Jumuiya ya wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania TAREA imetoa wito kwa makampuni ya nishati hiyo kuongeza wigo wa huduma hiyo kwenye maeneo yenye uhitaji na yale ambayo hayajafikiwa na umeme wa gridi ya taifa ili kuhakikisha watanzania wengi wanatumia nishati ya umeme kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Siito huo umetolewa na Naibu Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo Emma Laswai wakati alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa ubia wa Kampuni za huduma za umeme Jadidifu za Luminous Power Technologies ya India na Swaminath Trading Ltd ya Tanzania kwa ajili ya kushirikiana katika kusambaza vifaa na zana bora za kisasa katika kutoa huduma hiyo hapa nchini.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Biashara ya Kimataifa, Luminous Revanand Andhale, ameahidi kupitia ushirikiano huo wataingiza nchini bidhaa zenye ubunifu wa hali ya juu zilizotengenezwa kwaajili ya soko la Tanzania ambazo ni suluhisho la kudumu la upatikanaji wa nishati kwa Watanzania kwasababu kuna ongezeko la mahitaji ya umeme nchini na wanaiomani vitawafaa Watanzania kwa matumuzi ya kila siku.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Swaminath Group, Mayur Dilesh Solaki, amesema wataleta vifaa vya umeme mbadala vyenye viwango ubora wa kimataifa hii ikiwa ni dhamiria ya kuboresha teknolojia kwenye huduma ya nishati jadidifu kwa kutumia vifaa vyenye ubora ili kuhakikisha kwamba huduma inayotolewa inaendelea kuwa rafiki wa mazingira kama inavyosisitizwa kwenye malengo endelevu ya Taifa.