Serikali ya Jamhuri ya Burundi imezindua  ujenzi wa miundombinu katika eneo la Bandari kavu ya Kwala lililoko Mkoani Pwani.

Uzinduzi huu unaashiria kuanza rasmi kwa ujenzi wa Uzio Pamoja na miundombinu ya kibandari kwenye eneo la hekari 10 ambalo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) iliikabidhi  kwa Serikali ya Jamhuri ya Burundi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Waziri wa Uchukuzi wa Burundi Marie Chantal Nijimbere amesema uendelezaji wa Bandari kavu ni kiungo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi hizi mbili na uendelezaji wa biashara ya Kimataifa. 

Nijimbere amesema Bandari kavu itarahisisha uagizaji shehena bila muagizaji kwenda bandarini na badala yale atakuja katika Bandari kavu.

Akizungumza kwa Niaba ya Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Ally Possi amesema uzinduzi huo ni ishara ya kuendelea kwa mahusiano mazuri yanayolenga kukuza biashara na Uchumi baina ya nchi hizi mbili.

Amesema ujenzi wa miundombinu ya kibandari inaenda kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na ni hatua itakayopunguza gharama za usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Hasa Ushoroba wa Kati (Central Corridor). Amesema eneo la Kwala linauwezo wa.kuhifadhi zaidi ya makasha 30,000 kwa wakati mmoja.

Naye Katibu Mtendaji wa Taasisi ya kuwezesha Usafirisha wa Ushoroba wa Kati (Central Corridor), Wakili Flory Okandju, amezishukuru na Kuzipongeza nchi hizo wanachama wa Ushoroba wa kati kwa hatua hii muhimu ya Uzinduzi wa ujenzi wa Bandari kavu ya Burundi katika sehemu ya Kwala kwani ni hatua nyingine muhimu katika safari ya kuboresha utengamano wa Kikanda, kuboresha miundombinu ya Usafirishaji na kukuza biashara.

Ameongeza kuwa, taasisi ya Central Corridor ambayo ilifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa eneo hilo la Bandari Kavu ya Kwala, sasa itashirikiana na nchi ya Burundi katika ujenzi wa miundombinu yake ili iweze kuchangia katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kwa haraka na kwa uhakika zaidi, ikichangia kuongezeka kwa kiwango cha biashara na ukuaji wa uchumi unaounganisha mataifa yetu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA,Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano Dkt.George Fasha amesema lengo la kuanzishwa kwa Bandari kavu ya Kwala ni kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar-es-Salaam.

Aidha amesema watumiaji wa Bandari kavu ya Kwala watapata faida nyingi kama vile kupewa siku 60 za kuhudumia shehena.

Share with Others