Mfano wa skrini ya TV "unayoweza kulamba" ambayo inaweza kuwa na ladha ya chakula imetengenezwa na profesa wa Kijapani, Reuters inaripoti.
Katika teknolojia hiyo Inayojulikana kama Taste-the-TV, makopo kumi yananyunyizia ladha kwenye "hygienic film"(filamu ya usafi) ambayo inakunjwa juu ya skrini ili mtazamaji ailambe.
Profesa Homei Miyashita wa Chuo Kikuu cha Meiji, alisema kuwa TV ya aina hiyo inaweza kutumika kutoa mafunzo kwa wapishi au wahudumu wa mvinyo.
Iwapo itatengenezwa kibiashara, TV hiyo itagharimu $875 (£735), alikadiria.
"Lengo ni kufanya iwezekane kwa watu kukifahamu kitu kama kula kwenye mgahawa upande mwingine wa dunia, hata wakiwa nyumbani," aliiambia Reuters.
Anaripotiwa kuwa katika mazungumzo na watengenezaji kuhusu matumizi mengine ya teknolojia ya kunyunyizia ladha, kama vile kuongeza ladha kwenye mkate.