RAIS umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge , Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Dkt.Tulia Ackson amesema kuwa tani Mil.7 za uzalishaji wa taka ambazo zimekuwa zikizalishwa nchini ni asimilia 30 pekee ndizo zinafika Dampo hivyo ipo haja kwa wananchi kutumia kama fursa kwa kuanzisha viwanda vya uzalishaji wa malighafi.
Amesema kuwa kuna vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambao huwa wanaomba mikopo katika Halmashauri mbalimbali hapa nchini waweke mikakati ya kuomba mikopo hiyo ili waanzishe viwanda ambapo taka hizo zitakuwa fursa kubwa kwao kwa kuzibadili kuwa bidhaa.
Dkt.Tulia amesema hayo Juni 1,2024 wakati wa maadhimisho yla wiki ya mazingira kikanda ambapo kwa Mbeya yaliongozwa na Dkt.Tulia katika viwanja vya Kabwe Jijini hapa.
“Hizi taka zianze kuwa fursa kwenu nyie vijana, wanawake,na watu wenye ulemavu,nimesikia eneo la Mji Mdogo wa Mbalizi kuna kiwanda pale Mstahiki Meya wa Jiji yupo hapa sisi kama Jiji la Mbeya huwa tunatoa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye wenye ulemavu hivyo vikundi ambavyo huwa vinaomba mikopo kwa halmashauri hii ni fursa kwenu kuanza kutengeneza mazingira ili mtengeneze viwanda ambavyo vitakuwa vinatumia taka hizi ambazo wanazipata bure ili waweze kuziregeleza katika bidhaa ambazo wananchi wanaweza kuzitumia tena”amesema Dkt.Tulia.
Aidha Dkt.Tulia amesema kuwa Baraza la madiwani lipo tayari kuwaunga mkono katika hilo hivyo wakipeleka andiko linalohusu kuanzisha kiwanda watapata kwa ajili ya uregelezaji wa taka wataungwa mkono wa vifaa pamoja na mkopo .
“Hivyo naomba mtumie fursa hiyo ambayo inajitokeza kwenye ukusanyaji mzuri wa taka wa Jiji la Mbeya ili taka hizo muwe mnaletewa nyinyi harafu mnafanyia kazi ambayo itawaletea ajira na kuongeza kipato pamoja na kusogeza kimaendeleo kama Jiji la mbeya”amesema
Aidha Dkt Tulia alishukuru JKT kwa Kazi nzuri wanayofanya na mpaka Jiji kuchukua Tuzo ya usafi wa mazingira kwa kushika nafasi ya pili kati ya Majiji sita.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu (Mazingira)Ofisi ya Makamu wa Rais ,Christina Mndeme katika mwendelezo wa wiki ya mazingira nchi nzima amesema wanafanya usafi mikoa yote ikiongozwa na Makamu wa Rais Dkt.Philipo Mpango.
“Leo hii katika siku ya usafi tumewagawa katika Kanda tunayo kanda ya Mashariki inayoongozwa na Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango na Kanda ya Kaskazini inayoongozwa na Jaji Mkuu huku Kanda ya nyanda za juu kusini ikiongozwa na Spika wa Bunge na Rais umoja wa mabunge duniani na Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini Dkt Tulia Ackson katika viwanja vya kabwe Jijini hapa “amesema Mndeme.