SERIKALI imetangaza mkakati wa uboreshaji wa elimu nchini ambapo walimu ambao wataajiriwa ni wale wataokuwa wamefanya mitihani yao na kufaulu vizuri tofauti na ilivyokuwa awali wizara ilikuwa ikijaza nafasi zilizokuwa zikihitajika bila kupitia mchakato huo .
Profesa Mkenda ameyasema hayo jijini Tanga wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya hali ya ufaulu na ujifunzaji wa wanafunzi ulioshirikisha wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo Maofisa Elimu mikoa, Halmashauri,Wakurugenzi na Taasisi.
Amesema kwamba wanaona jambo hilo sio jema kwao lakini wajiulize kwanini madaktari wanapomaliza Shahada ya kwanza wanalazimika kufanya mitihani ndio wanafanya kazi hivyo suala hilo linapelekwa kwa walimu ili kuweza kupata walimu bora.
Profesa Mkenda amesema kwamba wanaamini kigezo hicho ndio ambacho kitalivusha taifa na watahakikisha wanachukua walimu waliobora zaidi na watakaofanya mitihani na kufaulu vizuri.
“Kama tunataka tuboresha elimu lazima twende kwa ujasiri tunapojaribu kuajiri Walimu tujiulize tunapigania mwanao apata Mwalimu bora sasa tutakapo ajiriwa lazima wafanye mtihani na watakaofeli hawatapata nafasi,”amesema.
Pia amesema Walimu waliopo watalindwa mpaka watakapostaafu na wataendelea kuwajengea uwezo kwani Rais anatenga fedha nyingi kwenye elimu.
“Tathimini tunayoifanya lazima iendelee na hatua nzuri za baraza hatufurahii kufutia mitihani watahaniwa na waliojaribu kuiba mitihani,”amesema .
Awali Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Caroline Nombo amesema taarifa ya tathimini ya ujifunzaji kwa wanafunzi wa kidato cha pili iliowasilishwa na Baraza la Taifa Mitihani (Necta) inatoa picha halisi kuhusu ufundishaji na ujifunzaji kwa shule za sekondari na msingi nchini.
Hivyo mapendekezo yaliyotolewa yanaonesha dira ya nini cha kufanya ili kuhakikisha ufundishaji,ujifunzaji na tathimini katika ngazi ya shule unaimarika.
Amesema Wizara hiyo itaendelea kushirikiana bega kwa bega na wadau wote wa elimu na baraza la mitihani kuhakikisha masuala yote ya ufundishaji na tahimini yanaimarishwa kwa lengo la kukuza umahiri wa wanafunzi katika masomo hayo.
“Wizara kupitia Baraza la Mitihani tutaendelea kuhakikisha kuwa tathimini ya ujifunzaji wa wanafunzi wa kidato cha pili awamu ya pili ya mwaka 2025 itafanyika kwa ufanisi mkubwa,”amesema
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani nchini (NECTA) Dkt Said Mohamed amesema suala la kufanya tathimini ni muhimu ili kuboresha kiwango cha elimu na wamekuwa wakifanya katika maeneo mbalimbali lengo ni kutaka kujua maendeleo ya wanafunzi wamesoma na wanataka kufika wapi.
Amesema wameanza kufanya tathimini kwa masomo manne ambapo wameanza Hisabati,Sayansi huku akieleza kwamba katika somo hilo katika mtihani wa darasa la saba mwaka huu utakuwa hauna maswali ya kuchagua.