Na Martha Magawa
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeadhimisha Siku ya Chakula Salama Duniani kwa kuendelea kusisitiza ulaji wa chakula salama kwa wananchi ili kuondokana na madhara ya kiafya na kiuchumi ikiwemo kushindwa kumudu katika biashra ya ushindani.
Hayo yamebainishwa leo Juni 7, 2024 Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi wakati akifungua mdahalo wa wadau katika kuadhimisha Siku ya Chakula Salama Duniani.
Amesema ulaji wa chakula kisicho salama umehusishwa na magonjwa mbalimbali, pamoja kusababisha changamoto nyingine za kiafya kama vile ukuaji duni kwa watoto, hali duni ya lishe kwa wakubwa na watoto, pamoja na kuongezeka kwa magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza.
Aidha, amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), inakadiriwa kuwa kila mwaka mtu mmoja katika kila watu kumi huugua kutokana na ulaji wa chakula kisicho salama duniani, na kuwa, watu 420,000 kati ya wanaougua hufariki.
"Wadau tunahimizwa kujenga uwezo katika kuzuia, kung’amua na kukabiliana na dharura zitokanazo na chakula kisicho salama. Kila mmoja katika nafasi yake analo jukumu la kufanya tathmini juu ya vihatarishi vinavyoweza kusababisha uchafuzi wa chakula na madhara yake, pamoja na kuweka miundombinu ya kukabiliana na hali hiyo, endapo ikitokea". Amesema Dkt. Katunzi.
Amesema Serikali kupitia taasisi zake imekuwa na mipango ya kukabiliana na vihatarishi vya usalama wa chakula na kuimarisha mfumo wa udhibiti wa usalama wa chakula, ikiwa ni pamoja na kuongeza ufuatiliaji na uratibu wa masuala mtambuka na kuimarisha mawasiliano kati ya serikali, wafanyabiashara wa chakula na jamii kwa ujumla.
Pamoja na hayo ameeleza kuwa ni wajibu wa wafanyabiashara wa chakula kuimarisha mifumo ya uzalishaji ili kuhakikisha uzalishaji wa chakula salama, kushirikishana uzoefu na kuimarisha mawasiliano kati yao na walaji.
Vilevile amesema walaji wanalo jukumu la kuelewa vihatarishi vya usalama wa chakula na mazingira yanayosababisha uchafuzi wa chakula, madhara yatokanayo na kula chakula kisicho salama, kutoa taarifa juu ya chakula kisicho salama, pamoja na kufahamu namna ya kukabiliana na matukio yatokanayo na ulaji wa chakula kisicho salama.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Chakula Salama kwa mwaka huu (Chakula Salama: Jiandae kwa usiyoyatarajia) inatahadharisha juu ya umuhimu wa kujiweka tayari wakati wote kukukabiliana na vihatarishi inayoweza kuathiri usalama wa chakula na pia utayari wa kukabiliana na madhara yatokanayo na chakula kisicho salama.