Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 lenye lengo la kutoa elimu juu ya Tanzania tuitakayo.
Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam Katibu Mtendaji Ofisi ya Rais-Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru, alisema kongamano hilo litafanyika Jumamosi ya tarehe 8 mwezi wa 6 ,2024 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwenye ukumbi wa mikutano Nkurumah
"Tunalo jukumu kubwa la kutoa elimu juu ya Tanzania tuitakayo 2050, ili kuwaandaa vyema wananchi wote kutoa maoni yao ambayo yanachangia kwa asilimia mia moja katika kuiandaa Dira 2050"
" Dira ya Taifa inapaswa kutupa picha ya matarajio ya nchi kufikia uchumi wa Juu wa Kati (High Middle Income Country) ifikapo mwaka 2050." Alisema
Mafuru aliwataka wananchi wote kushiriki katika kongamano hilo ili kutoa maoni yao na kuchangia katika mjadala mzima kuhusu Dira 2050.
Alisema wananchi hao wanaweza kushiriki kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu, majukwaa ya umma, tafiti, mijadala ya mitandao ya kijamii, na mikutano ya kijamii.
"Tume ya Mipango inasisitiza uelewa na hamasa kwa umma ili kila mtu ashiriki katika kutoa maoni yake. Tunatamani wananchi wote washiriki katika zoezi hili ili tuweze kujibu maswali mbalimbali ikiwemo Je, Dira 2050 inamtaka Mtanzania wa aina gani? Je, tunataka jamii ya aina gani ya Kitanzania ifikapo 2050? na Je, tunataka nchi ya aina gani ifikapo 2050?"
Mbali na hayo, Mafuru aliwataka waandishi kuendelea kuripoti juu ya Hatua zote za Maandilizi ya Dira 2050, kuandaa Programu za Elimu lakini pia Kutoa Majukwaa kwa Ushiriki wa Umma.