Takriban maafisa 2,000 wa polisi wa Kenya hawana uwezo wa kiakili kufanya kazi yao, mkuu wa huduma ya kitaifa ya polisi nchini anasema.

Inspekta Jenerali Hilary Mutyambai amesema hayo leo katika kongamano la maaskofu na makasisi wakuu akiongeza kwamba wamebaini visa hivyo "vya kushangaza" baada ya kuwafanyia uchunguzi wa kimatibabu maafisa wote wa polisi.

Kenya ina maafisa 100,000 wa polisi wanaofanya kazi chini ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi.

Ufichuzi huo unakuja huku kukiwa na ongezeko la idadi ya visa vya maafisa kujitoa uhai ndani ya jeshi la polisi.

Bw Mutyambai amesema shughuli ya kuwaondoa kazini baadhi ya maafisa wa polisi walioathiriwa imeanza kwa kuzingatia umuhimu wa kuwa na polisi walio sawa kiakili.

"Zana yetu ya kazi ni bunduki, na risasi moja inapotolpigwa, madhara yake ni makubwa," alisema.

Hata hivyo alisema mchakato wa kuwaondoa maafisa hao kazini sio rahisi kwa sababu ya taratibu za kina zinazohusika.

Kumekuwa na wasiwasi unaoongezeka katika miaka ya hivi karibuni juu ya afya ya akili ya maafisa wa polisi na serikali imekuwa ikisonga kushughulikia suala hilo.

Bw Mutyambai alisema kwa sasa polisi wana bodi ya kitaalamu ya afya inayojumuisha washauri na madaktari wa akili walioidhinishwa na wizara ya afya kutoa huduma za afya ya akili.

Kituo cha televisheni cha NTV kimeshiriki video inayaoangazia baadhi ya maelezo ya mkuu wa polisi:

Share with Others