Dar es Salaam. Mwanafunzi wa kidato cha pili (15) katika Shule ya Sekondari Chamazi amenusurika kuolewa baada ya Serikali kuingilia kati huku mumewe mtarajiwa, Maulid Athuman, mshenga na Sheikh wakikamatwa na Polisi.
Binti huyo anasema alikubali kuolewa ili kuepuka kero ya migogoro ya ndoa ya wazazi wake ambayo amekuwa akiishuhudia kwa muda mrefu, ingawa bado alikuwa akitamani kuendelea kusoma.
Wakati hilo likitokea, Serikali imesema itaanzisha mfumo wa kufuatilia ushughulikiaji wa matukio ya ukatili wa kijinsia yanayopokelewa ili wahusika wachukuliwe hatua haraka.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mbele ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maaalumu, Dk Dorothy Gwajima, Ofisa Ustawi Manispaa ya Temeke, Lilian Mafole alisema Aprili 14, 2022 mchana walipigiwa simu na msamaria mwema ikiwataarifu kuna mwanafunzi anatarajiwa kufunga ndoa Aprili 15, 2022 saa 2:00 usiku.
“Baada ya kupokea taarifa hiyo niliwasiliana na vitengo tofauti, tukafanya uchunguzi kujiridhisha na kuyafahamu vizuri mazingira ya tukio na tukafanikiwa. Siku ya tukio saa mbili usiku tulifika tukiwa na timu nzima akiwamo mkuu wa shule na polisi.
“Tulifanikiwa kuzuia ndoa hiyo kufungwa na watuhumiwa watatu wamekamatwa na kupelekwa kituo cha polisi kwa hatua za kisheria,” alisema Mafole.