Kufuatia unyakuzi wa kijeshi katika nchi tano tofauti za Afrika katika mwaka uliopita, baadhi wamependekeza kuwa demokrasia inaweza isiwe aina bora ya serikali katika bara hilo.
Lakini hapa, Leonard Mbulle-Nziege na Nic Cheeseman wanasema kuwa - licha ya vikwazo hivi - demokrasia ni njia ya kipaumbele kwa Afrika.
Afrika imekumbwa na msururu wa mapinduzi ambayo yanatishia kuirudisha nyuma miaka ya 1980 na enzi za utawala wa kijeshi.
Burkina Faso, Chad, Guinea, Sudan na Mali zote zimeshuhudia serikali ikipinduliwa na nafasi yake kuchukuliwa na jeshi.
Hali inaweza kuwa ya kutisha zaidi, kwa sababu majaribio yaliyofeli ya mapinduzi yameripotiwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na siku chache zilizopita, Guinea-Bissau.
Kwa kila nchi ambayo inaongezwa kwenye orodha hii, sauti zinazodai kuwa demokrasia haifanyi kazi - na haiwezi kufanya kazi - katika Afrika inakua zaidi.
Kwani, kupinduliwa kwa marais wa kiraia kulifuatiwa na sherehe za mitaani katika baadhi ya nchi huku wananchi wakishangilia kuangushwa kwa viongozi waliochaguliwa.